Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Kheri James ametoa wito kwa Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya kuwawezesha vijana kiuchumi ili kuwaepusha na makundi ya uhalifu katika jamii.
Akizungumza mjini Igwachanya, Wilayani Wanging’ombe mkoa wa Njombe wakati akiwa katika ziara ya ukaguzi wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kukagua miradi ya maendeleo ambapo amesema kama vijana hawatawezesha utekelezaji wa sera ya viwanda ambayo inatengeneza ajira za kujiajiri haitafikiwa.
Amesema kuwa lengo la Serikali hivi sasa ni kuhakikisha vijana nchini wanajengewa nguvu za kuweza kuzalisha na baadae kuwaajiri ili kukuza uchumi wa nchi na uchumi wao binafsi.
“Kama hatutawawezesha vijana wakamiliki uchumi, tutaua uchumi wetu,kwa sababu uchumi unakua kwa kuanza na uchumi mdogo mdogo, lakini pia kama hatutawawezesha vijana kundi la walalamikaji, watu ambao wanaona nchi inaendelea wengine wanafurahia wao wanaangamia,ile ndoto ya kutengeneza ajira ya watu kujiajiri itakuwa imekufa,” amesema James.
Amesema kwa vijana wengi wananguvu na akili lakini wakianzisha shughuli zao hazifiki mwisho na kufa na kwamba rais Magufuli ameelekeza na kusisitiza kote nchini halmashauri zote ziwezeshe vijana kupitia fedha za mikopo zilizopo hivi sasa.
Aidha, James amewataka Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya kuvisimamia vikundi vya ujasiriamali vilivyopo katika maeneo yao ili kuwajengea vijana uwezo wa kuinua vipato vyao kupitia viwanda vidogo vidogo wanavyovianzisha.
Amesema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inataka kuhakikisha inatengeneza mazingira wezeshi kwa watanzania walioamua kufanyakazi kwa maslahi ya taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Ally Kasinge ameahidi kutuma wataalam ili kuwasaidia wafugaji kupata taaluma ya uendelezaji wa miradi yao.
Naye Katibu wa CCM mkoa wa Njombe, Paza Mwamlima amewataka wanachama kutoa ushirikiano katika ukaguzi wa mali za chama katika maeneo yao.