Mwenyekiti Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe leo Julai 26, 2021 anadaiwa kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka ya ugaidi yanayomkabili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema inadai kuwa taarifa zaidi kuhusu sakata hilo, zitatolewa baadaye na chama hicho.
Kiongozi huyo wa chama hicho, kikuu cha upinzani nchini, alitiwa mbaroni alfajiri ya kuamkia Julai 21 akiwa hoteli ya Kingdom mtaa wa Ghana alikokifikia kwa ajili ya kushiriki kongamano la Katiba Mpya lililoandaliwa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).
Hata hivyo, siku iliyofuata Msemaji wa Polisi nchini, David Misime aliueleza umma kuwa Mbowe anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo za kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi na kuua viongozi wa Serikali.