Shirikisho la soka nchini TFF limeendelea kusisitiza mchezo wa kiungwa baina ya klabu za ligi kuu ambazo kwa sasa zinajipanga kupambana vilivyo, ili kuhakikisha zinatimiza malengo waliyojiwekea ya kutwaa ubingwa, kusalia katika ligi pamoja na kutokushuka daraja.

Katibu mkuu wa TFF Celestine Mwesigwa amesema wanataka kuona kila timu ikiwajibika kwa kufuata kanuni za soka zinazotambulika dunia, na katu hawatofumbia macho uchafu wowote ambao utakua na lengo la kuwakandamiza wachache.

Mwesigwa ameongeza kuwa, soka ni mchezo wa wazi na lolote litalofanywa kwa lengo baya, TFF pamoja na washirika wake wataliona, hivyo amesisitiza wadau wa mchezo huo kuwa makini.

“Tunataka kuona haki inatendeka katika michezo yote iliyobaki, kila mmoja aonyeshe uwezo wake kisoka na sio kutumia njia ambazo hazitakiwi katika mchezo wa soka, tunatoa tahadhari kwa yoyote atakaekwenda kinyume kwa kutaka kuudanganya umma, kwa kusema tutashughulika naye.”

Katika hatua nyingine Mwesigwa amezitaka klabu za Lipuli FC, Singida Utd na Mji Njombe, kujipanga vizuri kabla ya kuanza nginja nginja za ligi kuu msimu ujao.

Amesema klabu hizo zinapasa kufahamu ushindani madhubuti uliopo katika ligi kuu, hivyo viongozi pamoja na wadau wengine wanapaswa kuwa na malengo yanayofanana na sio kuelekeza nguvu zao kwenye migogoro.

Klabu za Lipuli FC, Singida Utd na Mji Njombe zimepanda kucheza ligi kuu, baada ya kufanya vyema katika mshike mshike wa ligi daraja la kwanza msimu wa 2016/17.

Shabiki Wa Lionel Messi Aichanganya Dunia
Live: Rais Magufuli akipokea taarifa ya vyeti kwa watumishi wa Umma