Kampuni ya Uwekezaji kwenye utalii na ranchi za wanyama, Mwiba Holdings Ltd imetishia kuwachukulia hatua kali za kisheria wanasiasa waliosambaza taarifa za uongo kupitia mikutano yao, wakidai walidanganya kuwa kampuni hiyo (na mmiliki wake Thomas Dan Friedkin), imepewa umiliki wa ekari milioni 6 za eneo la Hifadhi ya Wanyama Wilayani Meatu Mkoani Simiyu.
Kupitia mikutano ya hadhara ya kisiasa inayoendelea Kanda ya Ziwa, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu, alinukuliwa akitoa tuhuma hizo, zinazodaiwa kuwa ni za uongo, ambapo kwa mujibu wa takwimu za Mkoa wa Simiyu, mkoa mzima una eneo la kilomita za mraba 23,807 sawa na takribani ekari milioni 2.4. Eneo la Wilaya ya Meatu lililoko kwenye hifadhi ni kilomita za mraba takribani 4,253 sawa na ekari 425,000.
Katika taarifa yake kwa umma, Mwiba Holdings Ltd imesema haimiliki ardhi yoyote kwenye maeneo ya hifadhi nchini Tanzania na kwamba wilayani Meatu kampuni hii inafanya kazi kwa mikataba ya uwekezaji na upangishaji ambayo imeingia na Halamshauri za Vijiji ambazo ndizo zinazomiliki maeneo hayo. Jumla ya maeneo yote haya yaliyopangishwa ni ekari 171,604 – na si ekari milioni 6 kama ambavyo Lissu amekua akidai.
Kwa takwimu hizO, ina maana maelezo ya Lissu yanamaanisha Mwiba imepewa eneo ambalo ni mara 14 ya eneo lote la Hifadhi Wilayani Meatu, na mara tatu ya ukubwa wa mkoa wote wa Mkoa wa Simiyu – jambo ambalo linaonyesha dhahiri taarifa hizo kuwa si sahihi.
Aidha, kampuni hiyo (Mwiba Holdings) imeeleza kwamba haijaingia mkataba wowote na Serikali ya Awamu ya Sita kama inavyoelezwa na wapotoshaji, bali mikataba yake ya upangaji na uwekezaji kwenye maeneo haya imekuwepo kwa muda mrefu na iliongezewa muda mwaka 2018 na 2019 wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano.