Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema watu wanaofanya mauaji na kujificha kwenye kivuli cha ‘watu wasiojulikana’ siku zao zinahesabika  na wamefika ukingoni.

Amesema kuwa vyombo vya usalama nchini viko imara, vinafanya uchunguzi na vitawatia nguvuni watu hao hata kama siku yao itachelewa.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amejibu madai ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya kutaka uchunguzi wa tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu lichunguzwe na vyombo kutoka nje ya nchi.

Amesema kuwa hakuna sababu yoyote ya kutaka vyombo vya nje kuingilia uchunguzi wa suala la ndani kwani nchi ina vyombo vyenye weledi na uwezo mkubwa wa kufanya hivyo. Pia, Waziri Nchemba amesema hata kama watu hao wa nje wangeruhusiwa bado watawatumia wataalam wa ndani na watafanya kazi katika mazingira ya Kitanzania.

Alisisitiza kuwa uchunguzi hauwezi kukamilika ndani ya siku moja, hivyo watuhumiwa wa matukio ya mauaji na mengine ya kihalifu watatiwa nguvuni hata kama itachukua muda mrefu kama ilivyokuwa kwa Marekani kumsaka na mwisho kumuua kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda, Osama Bin Laden baada ya miaka 10.

“Nchi yetu inajitegemea, hakuna haja ya kuleta vyombo vya nje kufanya uchunguzi. Upelelezi utafanywa na vyombo vyetu. Watafikishwa kwenye vyombo vya humuhumu na watahukumiwa na watoto wetu,” amesema.

“Uchunguzi hauna ukomo, unaisha pale tu wahusika wote wanapokamatwa, vinginevyo uchunguzi hauishi. Maana hata Marekani walimtafuta Osama kwa muda mrefu sana hawakusema sasa tumesitisha kumsaka,” aliongeza.

Lissu anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya baada ya kushambuliwa kwa risasi Septemba 7 akiwa ndani ya gari nyumbani kwake mjini Dodoma.

Basi la Tashrif lateketea kwa moto Tanga
Nick Minaj akubali mziki wa Cardi B, ampongeza kwa kuvunja rekodi