Katika kuhakikisha kuwa haki ya Mbunge inalindwa wakati wa vikao vya Bunge vikiendelea, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amepiga marufuku Jeshi la Polisi Nchini kuwakamata wabunge wakiwa katika vikao vyao kwani kufanya hivyo ni kuchelewesha shughuli mbalimbali za Bunge.
Ameyasema hayo Mjini Dodoma wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge kuhusu Wizara yake, Nchemba amesema kuwa suala hilo limekuwa likiwasumbua wabunge kwani kufanya hivyo ni hatari na gharama ni kubwa za kuwasafirisha hivyo ameliagiza Jeshi hilo kutofanya hivyo.
Amesema kuwa wabunge wapo Bungeni hapo kwa shughuli za kitaifa na kuwakilisha wananchi wao, hivyo chombo chochote kinachotaka kufanya mahojiano na mbunge itakilazimu kifanyie mahojiano hayo hapo hapo bungeni.
“Chombo chochote kinchotaka kufanya mahojiano na wabunge, waje wafanyie hapa bungeni, wachukue maelezo yao hapa kwa waheshimiwa,”amesema Mwigulu.
Aidha, amesema kuwa uamuzi huo hauingilii masuala yanayohusu utaratibu wa kumkamata mbunge yaliyo ndani ya utaratibu wa Spika wa Bunge.
Hata hivyo, Mwigulu amesema kuwa Wizara yake inawajibu wa kuhakikisha haufanyiki uhalifu wa aina yeyote nchini na kuongeza kuwa nchi hii inaongozwa na utawala wa sheria hivyo hakuna mtu aliye juu ya sheria.