Naibu waziri wa fedha na mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba amekanusha tuhuma za kutoa rushwa katika mchakato wa kura za maoni unaoendelea jimboni kwake.

Nchemba ambaye alikuwa akihojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoani Singida, kwa tuhuma za kukiuka Sheria ya Gharama za Uchaguzi na  Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba Moja ya Mwaka 2007,  jana alijitokeza mbele ya waandishi wa habari na kueleza kuwa tuhuma zilizoelekezwa kwake na wagombea wenzake hazina ukweli na kwamba wagombea hao wamejaa uwoga wa kushindwa katika uchaguzi huo.

Akijibu baadhi ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili, Nchemba alisema kuwa kazi ya kandarasi ya kutengeneza mabarabara katika eneo hilo haikufanyika kwa kuwa yeye anagombea ubunge bali ni sehemu ya kazi za serikali.

Aliongeza kuwa shughuli hizo hazikuwa sehemu ya kuwashawishi wapiga kura wake kama ilivyoelezwa na walalamikaji na kwamba hiyo ilikuwa mipango ya kazi za halmashauri.

Mgombea huyo alijigamba kuwa hata kama asipofanya kampeni, wagombea wenzake hawana uwezo wa kumshinda katika kinyang’anyiro hicho na kwamba robo tatu ya wapiga kura tayari wanamuunga mkono.

Katika hatua nyingine, Nchimbi aliwapongeza Takukuru kwa hatua waliyochukua kumhoji akieleza kuwa walikuwa wanafanya kazi yao.

Awali, Mwigulu Nchemba alilalamikiwa na wagombea wenzake, David Jairo, Amon Gyuda na Juma Kilimbi walioileza Takukuru kuwa mgombea huyo alikuwa akitoa ahadi mbalimbali na kufanya baadhi ya shughuli kwa lengo la kuwashawishi wapiga kura. Pia walimtuhumu kuwa aligawa pikipiki na baiskeli kwa wanachama wa CCM huku akiwalaghai kwa hongo wasimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo.

Man Utd Wachezea Kichapo Marekani
Mwandosya Athibitisha ‘Kuponda’ Uamuzi Wa Kamati Kuu Ya CCM