Naibu Waziri Wa Fedha, Mwigulu Nchemba, amewataka watanzania kuhakikisha hawamchagui mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa kwa kuwa ni mmoja kati ya wagombea waliotumia fedha nyingi ili ahakikishe anaingia Ikulu.

Nchemba ameyaema hayo alipokuwa akihutubia umati wa wanachama wa CCM mkoani Mtwara, ambapo chama hicho kilitumia nafasi hiyo kumpigia debe mgombea wa chama chao, Dk. John Magufuli.

Alisema watu kama hao wanaotumia fedha, hukopa fedha nyingi ili kuhakikisha wanapata madaraka na kwamba huhangaika kwa kila hali ili kuhakikisha wanafanikiwa kupata namna ya kurejesha mkopo kupitia nafasi watakayopewa ya kuutumikia umma wa Watanzania.

“Kinachosumbua ni kwamba watalipaje madeni yale, maana yake wamewapa fedha hadi watoto wadogo ambao hawapigi kura. Sasa wanahangaika yale madeni watayalipaje, ndio maana wanafanya suala la urais ni la kufa na kupona,” alisema kada huyo wa CCM.

“Mimi nawaambia watanzania, kama tunataka utumishi tupeleke mtu ambaye hana madeni ya kulipa kwingine kokote zaidi ya kuwatumikia watanzania,” aliongeza.

Nchemba aliwataka watanzania kuwaogopa viongozi ambao wameihama CCM baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha kura za maoni kwa kuwa wameonesha dhahiri kuwa wanataka uongozi ‘kufa na kupona’.

Naye Dk. John Magufuli aliwahakikishia wananchi wa Mtwara kuwa atahakikisha anawatumikia vyema wananchi wote wa Tanzania kwa haki bila kuchagua chama japo anapitia CCM.

Siqueira Kujaribu Bahati Yake Juventus
Dr. Devota John Marwa Akatwa Na Kamati Ya TFF