Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba limefanikiwa kuupata mwili wa aliyekuwa askari wa kikosi cha KVZ Khalfan Junedi, aliyedaiwa kuuawa wiki tatu zilizopita eneo la Ngwachani Wilaya ya Mkoani.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba Ahmed Khamis Makarani amesema  pamoja na mwili huo, jeshi hilo pia limefanikiwa kuipata bunduki aina ya AK47 katika eneo la Ngwachani Novemba 12 majira ya saa 2:00 usiku huku magazine yake  ikiwa na risasi 21.

Kamanda Makarani amesema kuwa, Novemba 12 walifanikiwa kuupata mwili wa askari huyo baada ya kumkamata mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Ussi Foum Machano, mkazi wa Ngwachani, ambaye aliwapeleka kwenye eneo alilofukiwa na mwili huo ulipatikana katika kijiji cha Chonga kwenye bonde la Kisitu mbwa.

“Novemba 12 tulimkamata Ussi, maeneo ya Chake Chake, tulimhoji na ndipo akatuambia mahala ilipo bunduki na baadaye kwenda kutuonyesha eneo alipowekwa marehemu huyo”, amesema Kamanda Makarani.

Ameeleza kuwa, baada ya mwili huo kufanyiwa uchunguzi, walibaini kuwa marehemu  kabla ya kifo chake alikuwa na majeraha ya kupigwa huku akiwa amekatwa baadhi ya viungo vya mwili wake.

“Taratibu zote za kiuchunguzi kuhusiana na mwili zimefanywa, mwili umesafirishwa kwenda Unguja kwa ajili ya mazishi”, amesema Kamanda Makarani.

Kamanda Makarani amesema upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na watuhumiwa  watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika na kusema kuwa wanaamini watawakamata watu wengine waliohusika na tukio hilo.

Oktoba 28 mwa huu askari huyo pamoja na wengine walikuwa kwenye doria za kawaida, ambapo askari huyo alipotea majira ya saa 2:00 usiku akiwa na bunduki aina ya AK47.

Afrika Kusini yatoa hati ya kukamatwa kwa Mchungaji tajiri zaidi Afrika
De Bruyne: Kyle Walker hastahili lawama