Mwili wa aliyekuwa Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Christian Atsu Twasam, umerudishwa nchini kwao ukitokea Uturuki.
Atsu alifikwa na umauti katika tetemeko la ardhi lililotokea Uturuki majuma mawili yaliyopita, lakini mwili wake ulitolewa kwenye Kifusi juzi Jumamosi (Februari 18) chini ya nyumba yake kusini mwa Uturuki.
Ndege iliyobeba mwili wa marehemu ilitua mjini mjini Accra jana Jumapili (Februari 19) majira ya jioni, na jeneza lake lilibebwa na wanajeshi wa Ghana.
Akizungumza katika uwanja wa ndege wa Kotoka katika mji mkuu wa Accra, Makamu wa Rais wa Ghana Mahamudu Bawmia alisema: “Tulikuwa na matumaini dhidi ya matumaini, kila siku iliyopita, tulisali na kuomba.”
“Lakini alipopatikana akiwa amefariki.” Bawmia aliongeza kuwa mwanasoka huyo alipendwa sana na atakumbukwa sana. “Ni maumivu makali mno kumpoteza.” Na kuahidi kuwa Atsu atapewa mazishi “ya heshima”.
Kabla ya kufikwa na umauti Atsu, alikuwa naitumikia Klabu ya Hatayspor, inayoshiriki Ligi Kuu ya Uturuki.
Winga huyo aliichezea timu ya taifa ya Ghana mara 65 na kuisaidia timu yake kucheza mchezo wa Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2015.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 pia aaliwahi kucheza katika Ligi ya England akiwa na Klabu za Everton na Newcastle.