Baada ya faru Fausta ambaye anaaminika alikuwa ndiye faru mzee zaidi duniani kufariki jana akiwa na miaka 57, wizara ya maliasili na utalii imepanga kuutunza mwili wake kuwa kivutio cha utalii.
Naibu Waziri wa Utalii, Costantine Kanyasu, amesema baada ya Faru Fausta kufariki kama Wizara watashirikiana na baadhi ya wanasayansi ili kuangalia namna ya kuhifadhi mwili wa mnyama huyo ili Watalii waendelee kuja kumuona kama kivutio cha utalii.
Kwa mujibu wa taarifa ya upasuaji uliofanywa na jopo la madaktari wa wanyamapori na wataalamu wengine wa uhifadhi kutoka taasisi ya utafiti wa Wanyamapori nchini na hifadhi ya Ngorongoro, wamesema Faru Fausta alifikwa na mauti, baada ya moyo wake kushindwa kufanya kazi vizuri.
Faru huyo jike alikuwa chini ya uangalizi maalumu kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita baada ya afya yake kudhoofu na kuanza kushambuliwa na wanaya wakali mwituni.
Ikumbukwe kuwa mwaka Mwaka 2017 kulizuka gumzo kubwa mpaka Bungeni, juu ya gharama za matibabu na uhifadhi wa faru huyo baada ya kuwekwa kwenye uangalizi maalumu lakini mhifadhi mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) Dkt. Freddy Manongi amesema alisaidia kuingiza fedha pia.
“Suala la gharama ya matunzo wala halikuwa hoja kubwa, kwa mwaka mmoja toka Septemba 2017 alitumia milioni 16.2. Hauwezi kumuweka katika mazingira maalumu bila kutumia gharama…Lakini Hifadhi ya Ngorongoro inaingiza mapato yake kutokana na hawa hawa wanyama, mwaka jana pekee tumeingiza shilingi bilioni 143, lazima tuwatunze hawa wanyama,” amesema Dkt Manongi.
Nchini Tanzania Faru wanakadiriwa kuwa 200. Katika Hifadhi ya Ngorongoro kulikuwa na faru 108 mwaka 1968, idadi hiyo ikaporomoka mpaka 25 mwaka 1977 na hali ikawa mbaya zaidi mwishoni mwa miaka ya 80 ambapo walikuwa chini ya 10. Kwa sasa hifadhi hiyo ina faru zaidi ya 50.