Familia moja katika Kijiji cha Eburinde imeshangazwa na kitendo cha uongozi wa Kaunti ya Kakamega nchini Kenya kudai sare alizozikwa nazo ndugu yao.
Martin Shikuku Alikoye(31) aliyekuwa akifanya kazi kikosi cha ulinzi cha vijana wa kaunti ya Kakamega alifariki dunia baada ya kuzama kwenye maji wakati akivuka mto.
Aidha, uongozi wa Kaunti ya Kakamega ulifika nyumbani kwa marehemu na kuomba wapewe sare za kazi za marehemu, ndipo familia iliwaeleza kuwa kijana wao alizikwa na sare hizo ndipo ikatolewa amri ya kuufukua mwili huo ili sare zivuliwe.
”Tuliishirikisha kikamilifu serikali ya kaunti ya Kakamega katika mipango ya mazishi na hawakupinga pendekezo letu kumzika akiwa na sare za kazini,”amesema Francis Mutamba kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation.
Hata hivyo, ndugu wakiwa wamejawa huzuni walishuhudia mwili wa kijana wao ukifukuliwa na kuvuliwa sare ambazo zilichukuliwa na watumishi wa kaunti ya Kakamega.