Mwili wa mwandishi wa habari, Douglas David, aliyekutwa amefariki dunia chumbani kwake eneo la Vingunguti Mji mpya Jijini Dar es salaam, unatarajiwa kusafirishwa leo januari 28, 2020 kuelekea Sumbawanga mkoani Rukwa kwaajili ya mazishi.
Imeelezwa kuwa marehemu Douglas aligunduliwa amefariki na majirani zake baada ya kuhisi harufu kali kutoka chumbani kwake, ndipo wakafanya utaratibu wa kufungua mlango kwa kushirikiana na viongozi wa serikali ya mtaa chini ya usimamizi wa polisi kituo cha Buguruni.
Kamishna msaidizi wa polisi mkoa wa Ilala, Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa kifo hicho.
“Mwili wake ulikutwa umelala kifudifudi kitandani kwake ukiwa umeharibika tayari, majirani wanasema waliamua kuuvunja mlango baada ya kutomuona kwa siku tatu, lakini pia kusikia harufu iliyokuwa ikitokea chumbani kwake na wamesema marehemu alikuwa mgonjwa wa kifafa” amesema ACP Magomi.
Kabla ya kusafirishwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwaajili ya uchunguzi zaidi.
Hadi umauti unamkuta, Marehemu alikuwa akifanya kazi kwa kujitolea katika kituo cha TBC Online, kabla ya hapo aliwahi kufanya kazi katika vyombo vya habari vya Dar Mpya na Lemutuz Blog na tv online.