Klabu ya Geita Gold FC huenda ikaendelea kupata Pigo, kufuatia Mshambuliaji wake Daniel Lyanga kuhusishwa na Mpango wa kutimkia Dodoma Jiji FC katika kipindi hiki cha Dirisha Dogo la Usajili.
Geita Gold tayari imeshapata Pigo kwa kuondokewa na Wachezaji muhimu wawili Saido Ntibazonkiza aliyetimkia Simba SC pamoja na Yusuph Kagoma aliyetimkia Singida Big Stars FC.
Taarifa zinaeleza kuwa Uongozi wa Dodoma Jiji FC upo katika mazungumzo na Lyanga, na kama mambo yatakwenda kama inavyotarajiwa Mshambuliaji huyo ataihama Rasmi Geita Gold FC.
Mpango wa Dodoma Jiji FC kuwa mbioni kumsajili Lyanga, uliibuka kufuatia mapungufu ya safu ya Ushambuliaji ya Klabu hiyo yaliyonekana tangu mwanzoni mwa msimu huu, baada ya kuondoka kwa Anuary Jabir Muhajir, aliyetimkia Kagera Sugar FC.
Kufuatia kuondoka kwa Mshambuliaji huyo, kumeifanya safu ya Ushambuliaji ya Dodoma Jiji FC kufunga mabao 12 pekee katika Michezo 19, waliocheza hadi sasa.
Kocha wa timu hiyo, Melis Medo, amekuwa akiwatumia kinda Zidane Sireri, Collins Opare, Hassan Mwaterema, Christian Zigar na Paul Peter lakini timu hiyo ina changamoto ya ufungaji wa mabao.
Kutokana na hali hiyo, uongozi umeona kuna haja ya Medo kuongezewa wachezaji wa mbele ambapo mmoja ya viongozi wa juu wa timu hiyo ambaye anashughulikia usajili, amesema chaguo la kwanza la kocha ni Mshambuliaji Daniel Lyanga.