Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi amemtembelea Rais Samia Suluhu Hassan nyumbani kwake kwa lengo la kumjulia hali na kumtia moyo katika safari ya uongozi wa Taifa aliyoianza, huku akimpa ujumbe wa jinsi ambavyo watanzania wamempokea kwa furaha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Mzee Mwinyi amesema kuwa Rais Samia ameanza vizuri, watu wamempenda na kufurahishwa na hatua zake za awali na kwamba kama ungekuwa wimbo angeomba urudiwe.
“Mama ameanza vizuri. Ungekuwa ni wimbo ningesema ‘Once More’ (mara nyingine tena). Ameanza vizuri kabisa na kila mmoja ana furaha, kila raia aliyemsikia anasema ‘mama ameanza vizuri. Tuliyekuwa naye alikuwa rais mzuri sana na mzoefu wa mambo ya kiserikali, ametufanyia kazi nzuri sana, sasa kayaacha mambo haya ghafla kamuachia mwenzie” amesema Mzee Mwinyi.
“Sasa mama naye mwanadamu atakuwa na yake na vilevile kuna mambo ambayo yameanzwa na mtu mwingine ambayo watu wanayataka wanayapenda, wanamshikilia ‘Mama tunayataka haya tunayataka’, tulieni tutayatekeleza haya, sasa hilo linafurahisha,” ameongeza.
Aidha, Mzee Mwinyi amesema kuwa yeye pamoja na wazee wenzake wako tayari kumpa ushirikiano wakati wowote atakapohitaji.
Rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewataka wananchi kumuunga mkono Rais Samia kwa kuhakikisha wana umoja na mshikamano katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.