Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, amesema ugonjwa wa corona umekuwa kisingizio katika ukusanyaji wa kodi licha ya kwamba inaonyesha hakuna jitihada za makusudi kufikia lengo.

Akizungumza Ikulu Zanzibar alipofanya mazungumzo na uongozi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ukiongozwa na Gavana Prof. Florens Luoga.

Amesema licha ya kuwapo kwa ugonjwa wa corona, mifumo ya kodi nayo ikikaa sawa mafanikio makubwa yanaweza kupatikana na kutekelezeka.

Dk. Mwinyi amesema uteuzi wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango anayeshughulikia kodi na fedha, utasaidia na ni vyema kiongozi huyo akahakikisha katika muda mfupi mifumo inakaa sawa na kwa vile anatokea BoT ana matumaini makubwa kwamba atapata msaada kutoka benki hiyo.

Aidha Mwinyi amesema kuna haja ya kutafuta njia bora ya kuwasaidia wajasiriamali ambapo mikopo inayotolewa hivi sasa masharti yake ni magumu ndiyo maana wengi wao wanafeli, hivyo msaada wa BOT unahitajika ili kupata njia nzuri zaidi.

Naye Prof. Luoga ameeleza azma ya BOT ni kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha uchumi wa Zanzibar unaimarika zaidi.

Amesema uchumi wa Zanzibar umeendelea kukua kwa kiwango cha kuridhisha kwa wastani wa asimilia 6.8 kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita na kwamba sekta ya huduma ndiyo imekuwa ikichangia zaidi.

Unyanyasaji wa kijinsia umehamia mitandaoni
Mourinho: Harry Kane atawavaa Arsenal