Klabu ya Coastal Union ya jijini Tanga imefanikiwa kukamilisha usajili wa Kiungo Mshambuliaji, Lucas Kikoti kwa kandarasi ya miaka miwili akitokea Namungo FC.
Kikoti kiungo mwenye umri wa miaka 28 ni moja ya sajili kwa ajili ya kuboresha eneo la ushambuliaji lililosababisha msimu uliopita 2022/23 timu hiyo kumaliza msimu ikifunga mabao 25 huku 35 wakifungwa.
Habari kutoka ndani ya Wagosi hao zinaeleza kuwa usajili huo ni mapendekezo ya kocha wao mkuu Mwinyi Zahera aliyetambulishwa juma lililopita akichukua nafasi ya Fikiri Elias.
Mbali na Kikoti, pia wamemsajili Beki Abdallah Denis ‘Viva’ kutoka Mlandege inayoshiriki ligi kuu ya Zanzibar kwa kandarasi ya miaka miwili ikiwa na lengo la kuboresha eneo la ulinzi.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa timu hiyo, Omary Ayub amesema hawezi kuzungumzia lolote kuhusu usajili kwa sasa kwa kuwa bado wanaendelea na usajili hadi dirisha litakapofungwa.
“Bado tunafanya usajili siku sio nyingi tutatangaza usajili wetu walioingia na wote waliotoka, lakini kwa sasa Kuhusu kikosi chao kuanza mazoezi alisema Julai 20 wataingia rasmi kambini mkoani Tanga kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao 2023/24.