Kikosi cha Coastal Union kinarejea mazoezini kuendelea na Programu baada ya kupewa mapumziko mafupi, huku kocha mkuu Mwinyi Zahera akiweka wazi jambo analoenda kulifanyia kazi ni eneo la beki na ushambuliaji.
Coastal inarejea mazoezini tangu ilipocheza mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar iliotoka sare ya bao 1-1.
Kocha Zahera amesema hajaridhishwa na maeneo hayo, hivyo kipindi hiki kifupi atayafanyia kazi.
“Licha ya wachezaji kuonyesha utayari mzuri ila bado tumekuwa na changamoto kubwa kwenye maeneo hayo kwa sababu hatuna uwiano mzuri wakati wa kufunga na kuzuia, jambo ambalo sio zuri kwetu kwani tunahitaji kutengeneza timu imara,” amesema.
Zahera ameongeza kuwa wakati huu ambao hawana mchezo wa ushindani ndio watakaotumia kurekebisha kasoro ambazo anaamini zitaleta tija kikosini huku akiweka wazi usajili mpya hadi sasa umezaa matunda.
Katika michezo miwili ambayo kikosi hicho kimecheza kimeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu huku kikifunga mabao mawili.
Coastal ilianza msimu huu kwa kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Dodoma Jiji kisha kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar.