Benchi la Ufundi la Coastal Union chini ya kocha kutoka DR Congo Mwinyi Zahera umechimba mkwara mzito kuwa kuwepo kwa wachezaji wenye uwezo bora na wazoefu kama ilivyo kwa kiungo wake, Ibrahimn Ajibu ni miongoni mwa vitu vinavyowapa jeuri ya kufanya makubwa msimu huu 2023/24.
Coastal Union ambao wanatumia Uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga kwenye mechi za nyumbani msimu huu wamefanya maboresho kadhaa ikiwemo usajili wa Ajibu ambaye aliwahi kuwika Young Africans chini ya Zahera.
Kufuatia kusimama kwa ligi kupisha ratiba ya mashindano ya kimataifa, wachezaji wa timu hiyo wanaendelea na mazoezi kwa ajili ya ratiba ya michezo yao ijayo.
Zahera amesema wanatambua ushindani ni mkubwa uliopo msimu huu na wamejipanga kupata matokeo na kutamba kuwa hali ya wachezaji kwa ujumla ni nzuri.
“Ukiangalia kila timu inahitaji pointi tatu kwa kila mchezo, tutahakikisha tunapambana sana uwanjani ili kuweza kupata matokeo mazuri na tunaamini ingizo la Ajibu ni miongoni mwa silaha zinatuzotupa jeuri.”