Aliyekua Kocha Mkuu wa Young Africans Mwinyi Zahera amemkingia kifua Kiungo Ibrahim AJibu, ambaye anadaiwa kushuka kiwango tangu alipoondoka Simba SC na kuhamia Azam FC.
Ajibu alisajiliwa Azam FC Januari 2022 akitokea Simba SC ambako alikosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza chini ya Kocha Franco Pablo Martin aliyoondoka Msimbazi mwishoni mwa msimu uliopita.
Mwinyi Zahera ambaye aliwahi kufanya kazi na Ajibu aliposajiliwa Young Africans kuanzia mwaka 2017 hadi 2019 amesema bado anaamini Kiungo huyo ana uwezo mkubwa wa kucheza soka la ushindani lakini anakutana na mazingira ambayo sio rafiki.
Amesema ni kweli Ajibu ana mapungufu yake kama binaadamu, lakini kwa kocha yoyote anayefanya naye kazi hana budi kumvumilia na kutengenezea mazingira ambayo yatambadilisha ili aende sambamba na mfumo uliopo.
“Makocha wengi hawafahamu jinsi ya kuishi na Ibrahim Ajibu na akakupa kilicho bora. Chini yangu alikuwa anakuja mazoezini kwa kuchelewa, lakini nilivyokaa nae chini tukazungumza akawa anawahi mazoezi kuliko wachezaji wengine” amesema Mwinyi Zahera alipohojiwa EFM mapema leo Jumanne (Oktoba 18)
Mwinyi Zahera kwa sasa ni Mkurugenzi wa maendeleo ya Sokala vijana katika klabu ya Young Africans.