Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Klabu ya Young Africans Mwinyi Zahera, ametangazwa kuwa Kocha Mkuu wa Klabu ya Polisi Tanzania inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kabla ya kutangazwa kuwa Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania, Zahera alikua hana kazi kutokana na kumaliza Mkataba wake na Klabu ya Young Africans kama Mkurugenzi wa Maendeleo ya Soka la Vijana na Wanawake.
Zahera ametajwa kuchukua nafasi hiyo leo Ijumaa (Desemba 02), akichukuwa nafasi ya Kocha Joslin Sharif Bipfubusa kutoka nchini Burundi, aliyesitishsiwa mkataba wake mwezi uliopita.
Taarifa iliyotolewa na Polisi Tanzania FC na kusambazwa katika Mitandao ya Kijamii imeeleza kuwa, Kocha huyo kutoka DR Congo amejiunga na Maafande hao kwa Mkataba wa Miezi Sita, ambao utaisha mwishoni mwa msimu huu.
Pande hizi mbili zimefikia makubaliano ya Kusaini Mkataba huo, baada ya kufanya mazungumzo ya muda mrefu pamoja na tathmini ya kina ya kufanya vizuri kwa Timu ya Polisi Tanzania msimu huu.
Baada ya taarifa hiyo, Kocha Zahera alitambulishwa kwa Wachezaji wa Polisi Tanzania wanaoendelea na maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, utakaopigwa Uwanja wa Ushirika-Moshi Mkoani Kilimanjaro, Jumatatu (Desemba 05).