Mkurugenzi wa Soka la Vijana wa Young African, Mwinyi Zahera amesema Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele ana kila sababu ya kuwa Mfungaji Bora msimu huu, labda tu azembee mwenyewe.
Zahera ambaye amewahi kuwa Kocha Mkuu wa Young Africans, amesema Mshambuliaji huyo, ameonesha kuwa hana maskhara anapokua langoni mwa timu pinzani, hivyo hana shaka na kumaliza msimu akiwa kinara wa upachikaji mabao.
Amesema jambo kubwa ambalo linamuaminisha hivyo licha ya kuufahamu uwezo wa Mayele, ni uwepo wa wachezaji wengi kwenye kikosi cha Young Africans wanaoweza kutengeneza nafasi nyingi za kumuwezesha Mshambuliaji huyo wa zamani wa AS Vita kufunga.
“Yanga ina wapishi wengi wa mabao na Mayele naona kabisa ana kila sababu ya kuchukua tuzo hiyo na hata mwenyewe niliwahi kumueleza hivyo,”
“Mayele amekuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza anacheza zaidi ya dakika 80, kila mechi tena kwenye timu iliyoimairika kuanzia kipa hadi mbele, kazi ni kwake mwenyewe ila hakuna sababu ya kumzuia na kushindwa kufanya hivyo.” amesema Zahera
Hadi sasa Mayele ameshaifungia Young Africans mabao 09 katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akitanguliwa na Mshambuliaji wa Namungo FC Reliant Lusajo mwenye mabao 10.