Shirikisho la soka duniani  (FIFA), kwa mara nyingine, limeagiza klabu tisa za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na Klabu sita za Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes (TFDL) kujiunga mara moja na mfumo huo unaoitwa GPX yaani Global Players Exchange ambao malengo yake ni kurahisisha kufanya usajili kwa mchezaji.

FIFA imeiandikia barua Shirikisho la soka nchini (TFF), likitaja klabu tisa za VPL na TFDL kujisajili kabla ya Jumatatu wiki ijayo kwani itasaidia kupata taarifa kamili za mchezaji ambayo timu itahitaji kumsajili. Lengo ni kurahisisha mawasiliano ya usajili kwa mfumo wa Mtandao (TMS-Transfer Matching System).

FIFA imeleta tu orodha ya timu ambazo hazijajiunga, lakini TFF ikichambua majina hayo inaona kuwa majina ya klabu za VPL ni pamoja na African Lyon na Young Africans za Dar es Salaam, Mtibwa Sugar ya Morogoro, Ruvu Shooting na JKT Ruvu za Pwani, Mbeya City ya Mbeya, Ndanda ya Mtwara, Kagera Sugar ya Kagera na Mbao FC ya Mwanza.

Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes zimo African Sports na Coastal Union za Tanga, Marsh Athletic ya Mwanza, Friends Rangers ya Dar es Salaam, JKT Oljoro ya Arusha na Polisi Morogoro ya Morogoro.

Timu hizo hazina budi kujiunga na GPX hadi kufikia Jumatatu ya Septemba 5, mwaka huu. GPX ni kama mtandao wa kijamii unaoweza kulinganishwa na ‘WhatsApp’ unaofanya kuwa na mawasiliano ya karibu na FIFA imeagiza kuwa ni lazima mameneja wa TMS wa kila klabu na mashirikisho ya ya mpira wa miguu kujiunga na mtandao huo ambao si tu kwamba utafanya kazi katika nchi husika, bali pia unaunganisha ulimwengu wote.

Kwa mameneja wa usajili wa timu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes (SFDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL) watakaokuwa tayari basi hawana budi kuwasiliana na Meneja Usajili wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kupata maelezo ya kina ya namna ya kujiunga na mtandao wa GPX.

Hapi Awataka Watanzania Kulipa Kodi Kwa Wakati
Taifa Stars Kazini Kesho, Kuwakabili Nigeria