Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita amewataka Madaktari ,wauguzi pamoja na watoa huduma za afya katika Hospitali Vijibweni kutumia taaluma yao vizuri ili kuwawezesha wananchi wa eneo hilo kupata huduma nzuri.
Mwita ametoa ushauri huo jijini Dar es Salaam katika hafla iliyoandaliwa na wauguzi wa Hospitali hiyo iliyopo Wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam wakati walipokuwa wakiuaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka 2017.
Katika hafla hiyo pamoja na mambo mengine Mwita amesisitiza kwamba kila mmoja anapaswa kufanya kazi kwa upendo kwani kazi yao ni ya wito kuliko sekta nyingine.
“ Niko pamoja na nyinyi, najua kazi yenu hii ni ya wito, lakini mnaposhindwa kufanya kama ambavyo imekusudiwa hili ni tatizo, kwanini mpate sifa mbaya katika huduma yenu?” amesema Mwita.
Awali akisoma risala Dokta wa hospitali hiyo, amesema kwamba Hospitali hiyo inatoa huduma za rufaa kwa Kata za vijibweni ,Mjimwema, Kigamboni, Tungi, Somangila, Kibada na maeneo yote ya manispaa ya Kigamboni ambapo kwa sasa hospitali hiyo ndio inayofanya kazi za hospitali ya Wilaya katika manispaa ya Kigamboni.
Hata hivyo, amesema kuwa Hospitali hiyo inatoa huduma za wagonjwa wa nje (OPD) na ndani (IPD) pamoja na vipimo mbalimbali vya maabara na Ultrasound, Huduma za meno, Macho, Kisukari, huduma za maabara, baba na mtoto, magonjwa ya akili ,wagonjwa walio na maambukizi ya Ukimwi pamoja na mazoezi ya viungo.