Nini kinasababisha migogoro mahala pa kazi?

Ni kawaida kutumia muda wako mwingi kazini ukiwa na wafanyakazi wenzako kuliko familia au marafiki, na bahati mbaya wakati mwingine mnaweza msielewane. Kuna mambo mengi yanayoweza kusababisha kutokuelewana huku, mfano:

  • Umbea ofisini unaweza kusababisha kutokuelewana
  • Mawazo tofauti kuhusiana na kazi fulani
  • Namna tofauti za kujieleza
  • Hisia kali na jazba

Hata kama unadhani ni kosa lako au la, lililo sababisha mkanganyiko kati yako na mfanyakazi mwenzako, pale mkanganyiko huu unapoanza kuingiliana na utendaji kazi wako, ni wajibu wako kuondoa mkanganyiko huu. Hili linaweza kuwa jambo la kufadhaisha, haswa kama hupendi majibizano. Kwa bahati nzuri utatuzi wa migogoro ya kazini sio jambo linalohitaji majibizano.

Hatua hizi 5 zita kusaidia pale utakapokuwa na mgogoro na mfanyakazi mwenzako.

  1. Tambua tatizo

Njia rahisi ya kuondoa migogoro ni kukaa chini na kuzungumza. Lakini kabla hujaanza kuzungumza na mfanyakazi mwenzako, kwanza elewa ni nini ambacho kimekukera. Kwa mfano, kama mfanyakazi mwenzako alikuwa hasikilizi maoni yako kwenye utendaji kazi, au anakupatia kazi ngumu wewe tu, basi andaa mifano ambapo haya yalitokea. Hii itakuwezesha kueleza tatizo lako kwa ufasaha wakati wa mazungumzo. Kiujumla, inatakiwa ueleze kwa ufasaha tatizo kwa upande wako ni nini, ili mfikie muafaka kuhusu mabadiliko yanayotakiwa kufanywa ili kutatua tatizo hilo.

2.Usihamaki.

Pamoja na kutambua tatizo hasa ni nini, inabidi pia uondoe jazba wakati wa mazungumzo.  Hata kama mgogoro unahusiana na mambo binafsi zaidi kuliko kazi (mfano mfanyakazi mwenzako alikuwa anakusengenya), usichukulie kama jambo binafsi. Badala yake angalia ni namna gani tatizo hilo linaingiliana na utendaji wako wa kazi. Lakini kama una urafiki wa karibu na mfanyakazi huyo, hapo unaweza kulichukulia kama jambo binafsi na kulitatua kwa namna hiyo.

3.Ongeeni na msuluhishi

Namna nyingine ya kutatua tatizo ni kuomba mtu ambaye hahusiki na tatizo awasuluhishe bila upendeleo. Unaweza kuta na wewe umechangia kwenye kusababisha tatizo, hivyo inabidi ujirekebishe kwa namna fulani. Pia msuluhishi anaweza kuwapa namna ya kutatua tatizo ambayo hamkuifikiria hapo awali.

4.Pelekeni tatizo kwa Afisa Rasilimali Watu (HR).

Kama tatizo linaingilia utendaji kazi wako, au linahusisha bosi wako au mfanyakazi mwenye cheo kikubwa zaidi yako, basi ripoti tatizo kwa HR kwa njia ya maandishi. Na yeye itakuwa wajibu wake kulitatua. Ni kazi ya HR kuhakikisha kuwa mazingira yako ya kazi ni salama na yenye kuridhisha, hivyo usisite kumshirikisha kwenye utatuzi wa tatizo lako.

5.Samehe.

Wakati mwingine si vizuri kukuza kila tatizo dogo linalotokea kati yako na wafanyakazi wenzako. Kama hauna ukaribu, au haufanyi kazi na mfanyakazi huyo mara kwa mara, hii ni njia bora zaidi ya kutatua mgogoro kati yenu.

Sisi sote ni viongozi mahala pa kazi

Hata kama wewe sio bosi, inatakiwa tabia yako iwe ya kutolewa mfano mahala pa kazi. Hivyo usikubali migogoro yoyote ya ofisini ibadilishe tabia yako. Tatizo linapotokea litatue kwa kufuata utaratibu.

Lakini pia kumbuka, pamoja na kutatua tatizo fanya mabadiliko ili kuhakikisha halitokei tena.

 

MNH wazungumzia afya ya Kigwangalla, ujumbe kwa wanahabari
Ricardo Rodriguez kuziba pengo Arsenal