Mwenyekiti zamani wa Simba, Hassan Dalali jana Jumatatu, alipata ajali ya kuangushwa na bodaboda kwenye korongo, akitokea Uwanja wa Benjamin Mkapa, kushuhudia timu yake ikicheza dhidi ya Dodoma Jiji, iliyochapwa mabao 2-0.
Binti yake anayejulikana kwa jina la Umi Dalali, amesema baba yake alipoteza fahamu baada ya kuangukia kichwa kilichokuwa kuvuja damu, bodaboda akikimbia hivyo aliokolewa na polisi.
“Ajali alipatia Rangi Tatu njia ya kuingilia Chamanzi, polisi ndio waliomtambua baada ya kumfikisha kituoni, wakatupigia simu kwamba tukutane katika hospital ya Zakiem ambako alipatiwa huduma ya kwanza.” amesema Umi na kuongeza.
“Baada ya kutibiwa tukarejea nyumbani saa 8:00 za usiku, kwani ile hospitali hawalazi lakini asubuhi hali yake ilibadilika na sasa tupo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.”
Amesema ni ngumu baba yake kukaa nyumbani inapotokea Simba inacheza Dar es Salaam, amesisitiza ni kawaida yake kwenda kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wachezaji.
“Baba yangu anapenda sana Simba, asilimia kubwa ya muda wake aliutoa kwa klabu hiyo, imekuwa ngumu sana kwake kubaki nyumbani kama timu ikicheza Dar es Salaam.” amesema.
Chanzo: Mwanaspoti