Wakati uongozi wa Simba chini ya Rais Evans Aveva, ukionesha dalili za kukubaliana na ombi la bilionea, Mohammed Dewji ‘MO’ kuichukua klabu hiyo kwa ununuzi wa hisa, bodi ya udhamini imekuja juu na kupinga hilo.
MO ameweka bayana nia yake ya kuwekeza bilioni 20, kwa ajili ya kurejesha hadhi ya Simba ikiwa haijashiriki michuano ya kimataifa miaka minne sasa.
Aveva alikiri kuwepo na mpango wa MO, lakini akasema kuwa suala hilo linahitaji mchakato mzito mpaka kumfikia maamuzi ya kumpa mamlaka tajiri huyo.
Alisema mojawapo na hatua ni kujadili kwa kina thamani ya timu kisha kulifikisha kwa bodi ya wadhamini kabla ya kuliacha mikononi mwa wanachama katika mkutano mkuu ili kuridhia uwezekano wa kumuuzia hisa za umiliki wa timu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini, Mzee Hamisi Kilomoni, ametoa rai mapema kuwa mpango wa kuiachia timu hiyo kutoka mikononi mwa wananchi hauwezekani kwa hoja yoyote ile.
“Kwanza tangu Aveva aingie madarakani sijawahi kumuona na hajawahi kuonana na kiongozi yeyote wa bodi ya udhamini…MO yeye namsikia tu kwenye vyombo vya habari.
“Hatuko tayari kuiachia timu kwa vyovyote itakavyokuwa, hatuko tayari kuachia timu iwe mikononi mwa mtu mmoja kwa ushawishi wa milioni ngapi…kumbuka hawa wanakuja na kuondoka, sisi tuko palepale na sisi ndiyo wenye hati ya kufanya hivyo (kuidhinisha).
“Siafiki uwekezaji unaozungumzwa, si sahihi  na haujafuata misingi sahihi, vinginevyo tutaitelekeza timu kwa ushawishi wa bilioni 20 za mtu,” alisema mchezaji huyo mwasisi.
Wakati wengi wakiunga mkono adhima ya MO, kwani timu haina cha kujivunia miaka 80 sasa licha ya kuwa chini ya miliki ya wanachama, Mzee Kilomoni alifunguka: “Siyo kweli tuliingia Simba haina jengo, leo hii ina majengo mangapi, uwanja upo lakini wa kulaumiwa ni viongozi wanaongia madarakani mara kwa mara wanashindwa kuuendeleza siyo kweli kwamba timu haina kitu.”
Taarifa hii Kwa hisani ya Salehjembe

Samatta Asaka Baraka Za Serikali Kabla Ya Kwenda Nigeria
Rais Wa TFF Afunga Mwaka 2015 Kwa Zawadi