Kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru amezungumzia taarifa za kuvuliwa Ukamanda wa UVCCM Taifa kupitia kikao rasmi cha umoja huo.

Akizungumza na mwandishi wa habari wa gazeti moja kubwa kwa njia ya simu, Mzee Kingunge alionesha mshangao na kudai kuwa hajapata taarifa hizo.

“Wamenivua.. ?! Sijapata taarifa zozote, ndio kwanza nasikia kutoka kwako,” alisema Mzee Kingunge. Hii inaonesha kuwa hadi kufikia jana kada huyo mkongwe hajapata barua rasmi ya uamuzi wa UVCCM.

Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Sixtus Raphael Mapunda, alieleza kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa Baraza Kuu la umoja huo lilifanya mkutano Agosti 15 mwaka huu na kuamua kumvua Ukamanda Mkuu Taifa, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru kutokana na kutoridhishwa na mienendo yake ndani ya chama.

Moja kati ya vigezo vikubwa vilivyotumika ni pamoja na kutokuwa na imani na Mzee Kingunge kutokana na ukaribu wake na mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa pamoja na kukiuka baadhi ya misingi ya chama hicho.

Mzee Kingunge aliwahi kuzungumza na vyombo vya habari akipinga na uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM kulikata jina la Edward Lowassa katika mchakato wa kumpata mgombea urais wa chama hicho. Kada huyo alisema kuwa Kamati ya Usalama na Maadili inayoongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Dk. Jakaya Kikwete imekosa maadili.

 

 

BASATA Yalitoa Kifungoni Shindano La ‘Miss Tanzania’
Di Maria Uso Kwa Uso Na Mashabiki Wa PSG