Mwanasiasa mkongwe na mmoja kati ya waasisi wa TANU na CCM aliyetangaza kuachana na chama hicho hivi karibuni, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru amepanga kupanda rasmi kwenye jukwaa la Ukawa, leo jijini Arusha kumnadi mgombea wa Chadema, Edward Lowassa.

Taarifa za Kingunge kumnadi rasmi Lowassa leo, zimethibitishwa na meneja wa kampeni wa Chadema, John Mrema.

“Kesho (leo) Kingunge atangumza na watanzania kueleza kile anachokiamini, anataka mabadiliko, cha muhimu ni ujumbe wake,” Mrema anakaririwa.

Mzee Kingunge alitangaza kuachana na CCM kwa madai kuwa chama hicho kimepoteza muelekeo na kuvunja katiba yake. Alieleza kuwa utaratibu uliotumika kumpata mgombea urais wa chama hicho kupitia vikao vya Kamati ya Maadili na Usalama vilienda kinyume na taratibu na katiba ya chama hicho kwa maslahi ya viongozi wachache.

Hata hivyo, Mwanasiasa huyo mkongwe alieleza kuwa hatajiunga na chama chochote kwa hivi sasa lakini atabaki kuwa upande wa wale wanaotaka mabadiliko na kuiondoa madarakani serikali ya CCM.

 

Lowassa: Nimewaona CCM WakipitaPita Monduli…
Mvua Yaharibu Mchezo Wa Kihistoria