Mzee wa miaka 70 amekamatwa nchini Uganda kwa tuhuma za kulipiga mawe gari ya Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni likiwa kwenye msafara mwaka jana.

Mzee huyo ambaye amefahamika kwa jina la Omar Risasi Amabua alikamatwa katika Mji wa Arua na baadaye kuhamishiwa katika mahabusu iliyopo Gulu nchini humo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Nile Magharibi, Christopher Barugahare, amesema kuwa mtuhumiwa huyo atashtakiwa kwa uhaini na kwamba inatakiwa liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.

”Tumemkamata kwa sababu amehusishwa na tukio la mwaka jana ambapo gari la rais lilishambuliwa kwa mawe, na kwasasa sheria inachukua mkondo wake kwa wale wote waliohusika na tukio hilo,”amesema Barugahare

Aidha, gari hilo la rais Museveni lilishambuliwa Augosti 13, 2018, siku ya mwisho wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Manispaa ya Arua, kiti ambacho kiliachwa wazi kufuatia mauaji ya kinyama ya Mbunge, Ibrahim Abiriga na mlinzi wake ambaye alitajwa kuwa ni ndugu yake.

Rais Museveni alikuwa mjini Arua, siku ya mwisho wa kampeni ya uchaguzi mdogo, kumpigia debe mgombea wa NRM, Nusura Tiperu ambaye alishindwa katika uchaguzi huo na hata rufaa aliyowasilisha mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo ilitupiliwa mbali.

Kwa mujibu wa maafisa wa Ikulu ya Uganda na maafisa wa polisi, gari lililokuwa limebeba mzigo wa rais lilipigwa mawe na wafuasi wa upinzani, jambo ambalo halikubaliki, hali ambayo ilivifanya vikosi vya usalama kuingilia kati kutuliza mambo, ambapo watu 36 walikamatwa miongoni mwao wabunge na wanahabari.

 

TID akiri kuwaangusha mashabiki, 'Naombeni mnisamehe sana'
Vigogo 11 waikimbia nchi, Mbunge ang'aka maiti kutozwa fedha hospitali