Uongozi wa Chama cha Soka mkoani Mwanza ‘MZFA’ umethibitisha kufanywa kwa Maboresho/Marekebisho katika baadhi ya maeneo ya Uwanja wa CCM Kirumba, sambamba na chumba cha matibabu upande wa Mashabiki.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya ‘MZFA’ Kelvin Chela amesema wamekua na ushirikiano mzuri kati yao na wamiliki wa Uwanja, ambao ni Chama cha Mapinduzi ‘CCM’ katika kufanikisha kazi ya Maboresho hayo, kwa kuzingatia maagizo ya TFF.
“Tumefanya kazi hii kwa ushirikiano mkubwa na wamiliki wa Uwanja huu, tuliafikiana kuwepo kwa chumba maalum kwa ajili ya matibabu upande wa Mashabiki watakaofika hapa kushuhudia mchezo kati ya Simba SC dhidi ya Young Africans.”
“Marekebisho yaliyofanywa kwenye chumba hicho yanaridhisha kwa sababu, kilikua hakina hadhi hapo kabla, siku ya mchezo chumba hiki kitatumika, lakini kitaanza kutumika katika mchezo wa keshokutwa Jumapili kati ya Simba SC dhidi ya Geita Gold, na pia kitatumika katika mchezo wa Biashara United dhidi ya Young Africans.” amesema Kelvin
Simba SC ilitinga Nusu Fainali Kombe la Shirikisho kwa kuichapa Pamba FC ya Mwanza mabao 4-0, huku Young Africans ikiifurusha Geita Gold FC kwa changamoto ya Penati baada ya timu hizo kufungana 1-1 ndani ya dakika 90.