Kuna uwezekano AI Itihad yo Saudi Arabia ikarudi tena mezani katika dirisha lijalo la majira ya baridi ili kumsajili Mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah, ambaye ilishindwa kumchukua kwenye dirisha lililopita.
Tetesi za Salah mwenye umri wa miaka 31 kuhitajika Itihad zimechochewa sana na Mkurugenzi wa Mpira wa Miguu wa Ligi Kuu ya Saudia, Michael Emenalo ambaye ameweka wazi kwamba anatamani winga huyo mkali asajiliwe nchini humo.
Mkataba wa Salah unatarajiwa kumalizika ifikapo 2026. Al Ithad ilimuwekea dau la mshahara wa zaidi ya Pauni 150 milioni ili akubali kutua Saudia katika dirisha lililopita.
Liverpool haikuwa tayari kumuuza wakati huo na moja ya sababu kubwa ilikuwa ni muda mtupi wa kutafuta mbadala wake.
Moja ya sababu zinazofanya vigogo wa Saudia kutokata tamaa ya kumsajili ni asili yake ambapo wanaamini akitua kwenye ligi yao atavutia kundi kubwa la Waarabu.
Salah mwenyewe anadaiwa kuwa tayari kuondoka ingawa anataka kusubiri hadi mwisho wa msimu ikiwa ni sehemu ya kuonyesha heshima kwa Liverpool.