Mwanasiasa mkongwe nchini, Dkt. Chrisant Majiyatanga Mzindakaya amefariki dunia jana jioni alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam.

Mzindakaya alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo, hivyo kufanyiwa upasuaji na kulazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa zaidi ya wiki tatu sasa.

Mzindakaya alijizolea sifa hasa katika miaka ya 1990 kutokana na umahiri wake wa kuibua hoja na tuhuma ambazo zilitikisa zaidi kwenye Serikali ya awamu ya tatu iliyokuwa ikiongozwa na Hayati Benjamin Mkapa kiasi cha kupachikwa jina la `mzee wa mabomu’.

Katika kipindi hicho aliibua tuhuma za rushwa katika masuala ya mafuta, minofu ya samaki na sukari na kumfanya kujizolea sifa katika medani ya siasa nchini.

Wakati wa uhai wake, Mzee Mzindakaya alishika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM ikiwemo nafasi ya Ubunge katika jimbo la Kwela wilayani Sumbawanga ambako alidumu katika nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka 45 hadi alipostaafu siasa za majukwani mwaka 2010.

Aliingia bungeni tangu mwaka 1965 akiwa Mbunge wa jimbo la Ufipa Kusini, lakini mwaka 1981 Mahakama ilimvua Ubunge mwaka 1980 kwa madai ya kukiuka utaratibu za uchaguzi.

Hata hivyo, mwaka 1982 alirejea bungeni baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, kwani wakati huo wakuu wa mikoa walikuwa wakiingia bungeni moja kwa moja.

Aliendelea na wadhifa wa ukuu wa mikoa kwa miaka 13 kati ya mwaka 1982 hadi 1995 katika mikoa ya Mbeya, Morogoro, Kigoma na Rukwa.

Mwaka 1995 alirudi tena kwenye kinyang’anyiro cha ubunge baada ya kuombwa na wazee wa mkoa huo.

Katika nafasi ya Ubunge alishaongoza Majimbo ya Sumbawanga Mjini, Nkasi na Kalambo wakati huo likijulikana kama Sumbawanga vijijini.

Pia, aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara kwa miaka tisa na Mwenyekiti wa kwanza wa bodi ya Shirika la Viwanda Vidogo (Sido).

Atakumbukwa kwa kujenga hoja kali bungeni kiasi cha kusababisha baadhi ya Mawaziri kujiuzulu.

Katika awamu ya tatu ya Rais msaafu Benjamin Mkapa, Mzindakaya aliibua kashfa ya mafuta ya kula na suala la minofu ya samaki lililosababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Profesa Simon Mbilinyi na Naibu wake, Kilontsi Mporogomyi.

Pia aliibua kashfa ya sukari iliyosababisha aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Idd Simba naye kuachia ngazi.

Mzindakaya amefariki akiwa na umri wa miaka 80 na alizaliwa Desemba 31, 1940 mkoani Rukwa.

Bomba lapasuka, maji kukosekana kwa saa 24
Majaliwa awataka wananchi kuwa walinzi wa vifaa vya ujenzi