Baada ya kucheza michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kuambulia ushindi uliompa alama sita, Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi, ameonesha kutokua na mashaka na maendeleo ya kikosi chake ambacho awali kilitajwa kuwa na changamoto ya kukosa muunganiko.
Young Africans ilipata matokeo mabaya katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Zanaco FC ya Zambia (Siku ya Mwananchi), kisha ilipoteza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria, na sababu kubwa ya kiufundi ilitajwa ni ukosefu wa muungako wa kikosi cha Mwananchi.
Mtu wa karibu na Kocha Nabi amefichua siri hiyo kutoka ndani ya Kambi ya Young Africans, huko Avic Town, Kigamboni, Dar es Salaam, ambapoa mesema kocha huyo ameanza kufurahia muunganiko uliopo kwenye kikosi chake na kubainisha kwamba, suala la kupata ushindi katika mechi zao lina asilimia kubwa.
“Kwenye maelezo ya kocha baada ya mchezo wetu na Kagera Sugar, alionekana kuwasifu sana wachezaji wote wakiwemo viungo kama Fei Toto, Khalid Aucho na washambuliaji baada ya kuonekana kuunganika kwa haraka tofauti na matarajio yake.
“Pamoja na muunganiko huo, kocha amesema bado kuna dosari kidogo katika eneo la kutoa pasi za mwisho kwani anahitaji mashambulizi ya haraka wanapokaribia ndani ya 18, jambo ambalo kwake anaamini ndani ya mechi tano zijazo atakuwa ameshaanza kupata kile anachohitaji,” kimeeleza chanzo hicho.
Mbali na ushindi wa michezo ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar na Geita Gold, Young Africans ilifungua msimu kwa kuibanjua Simba SC bao 1-0, katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Septemba 25 Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.