Kocha Mkuu wa Young Africans Nesreddine Mohammed Nabi, amesema wachezaji wote wako katika hali nzuri kuelekea mchezo wa Mzunguuko wa saba wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya Kwanza FC.
Nabi ametangaza hali ya wachezaji wake baada ya kuwasili Jijjini Mbeya Jana Jumapili (Novemba 28) tayari kwa mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza FC utakaopigwa kesho Jumanne (Novemba 30), Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine.
Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema wamejiandaa vizuri kuelekea mchezo huo, huku wakitambua sehemu ya kuchezea ya Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine sio rafiki kwa kikosi chake.
Amesema amejiandaa kuikabili changamoto hiyo ya sehemu ya kuchezea ya Uwanja huo, sambamba na kuyafanyia kazi mapungufu baadhi ya makosa ambayo yalijitokeza kwenye mchezo uliopita dhidi ya Namungo FC uliomalizika kwa sare ya 1-1.
“Tumepata siku za kutosha kurekebisha mapungufu yote ambayo yalitupa changamoto, lakini pia wapo wachezaji ambao tuliwakosa kutokana na maumivu na wakati huu tutakuwa nao,” amesema Nabi.
Young Africans bado inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 16, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 14 huku Mbeya Kwanza FC ikiwa nafasi ya tisa kwa kumiliki alama 7.