Kocha Mkuu wa Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara Young Africans Nesreddine Nabi hatokuwa sehemu ya msafara wa klabu hiyo utakaoelekea Zanzibar leo Jumatatu (Januari 03).

Young Africans itaondoka Dar es salaam kuelekea Zanzibar tayari kwa utetezi wa Kombe la Mapinduzi walilolitwaa mwaka 2021 mbele ya watani zao Simba SC.

Taarifa kutoka Young Africans zinaeleza kuwa, Kocha Nabi ameondoka jana Jumapili (Januari 02) kwenda Ubelgiji iliko familia yake huku akipewa baraka na uongozi wa klabu yake.

Kocha huyo mwenye asili ya Tunisia, anarejea kwake kwa mapumziko ya siku 10 kukutana na familia yake ambayo hajaonana nayo kwa miezi mitano mfululizo.

Kocha Msaidizi Cedric Kaze anatarajiwa kuliongoza Benchi la Ufundi la Young Africans katika kipindi chote cha Michuano ya Mapinduzi 2022.

Kocha Kaze aliiongoza Young Africans mwaka 2021 kwenye michuano hiyo na kufanikiwa kutwaa ubingwa kwa kuichapa Simba SC kwa changamoto ya mikwaju ya Penati.

Mmoja kuondoka Young Africans kwa mkopo
Simba SC yaelekea Zanzibar