Licha ya kutapakaa kwa taarifa huenda akatimuliwa kazi na nafasi yake kujazwa na Kocha wa Mabingwa wa Uganda Vipers SC, Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi amejitokeza hadharani na kuzungumza na Waandishi wa Habari.
Nabi anatajwa kuwa kwenye wakati mbaya ndani ya klabu ya Young Africans, kufuatia kushndwa kufanya vizuri katika Mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan, kwa kushuhudia kikosi chake kikitupwa nje ya Michuano hiyo.
Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amezungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC FC, ambao utaunguruma kesho Jumatano (Oktoba 26), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Nabi amesema yupo tayari kwa mchezo huo ambao anaamini utakua mgumu na wenye ushindani mkubwa kutokana na kuimarika kwa kikosi cha wapinzani wake (KMC FC), ambao wametoka kuifunga Azam FC.
“KMC FC ni timu nzuri tunapaswa kuwaheshimu. Wameonesha upinzani mzuri kwenye mechi zilizopita bila shaka ufanisi wao ni mzuri. Tuna muda mchache wa kujiandaa lakini alama tatu kwetu ni muhimu”
“Tupo tayari kwa mchezo wetu wa kesho, tutaingia kivingine tofauti na tulivyoonekana kwenye mchezo uliopita dhidi ya Simba SC, naamini hata wao (KMC FC) wamejiandaa, hawatokuja kama walivyocheza mara ya mwisho dhidi ya Azam FC, tutapambana nao.”
Kocha Azam FC aitumia salamu Simba SC
“Tunafahamu kuwa ratiba yetu ni ngumu, tunafanya kila jitihada kuendana na uhalisia unaotukabili kwa sasa. Tuna michezo mingi na migumu mbele yetu na huo ndio ukweli ambao tunapaswa kupambana nao. Sio suala la nani atacheza ni suala la alama tatu” amesema Kocha Nabi
KMC FC inakwendea kucheza na Young Africans katika Uwanja wa ugenini, huku ikiwa na kumbukumbu ya Ushindi wa 2-1 dhidi ya Azam FC, huku Young Africans ikikumbukia sare ya 1-1 dhidi ya Simba SC.