Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Nasreddine Nabi amewakumbusha wachezaji wake kwa kuwaambia wasizidishe furaha ya ushindi uliowapeleka Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika, kwani bado wana kibarua kigumu cha kutetea Ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Kocha huyo kutoka nchini Tunisia ametao kauli hiyo baada ya kikosi chake kujihakikishia kucheza Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika jana Jumapili (Machi 19) kwa kuichapa US Monastir 2-0, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Nabi amesema wana muda mchache wa kushangilia kutinga Hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika, ili waendelee na majukumu mengine ya kutetea Ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ msimu huu 2022/23.
“Kila mchezaji wangu anafahamu umuhimu wa kila mchezo wa Ligi Kuu na michuano ya ASFC ili kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu.”
“Ni kweli tumeshinda dhidi ya US Monastir, lakini hii haitupi nafasi ya kuendelea kushangilia hadi kusahau majukumu mengine yanayotukabili katika kipindi hiki, tuna jukumu zito sana mbele yetu.”
“Haitakuwa kazi nyepesi kwetu kufanikisha hayo, ni lazima wachezaji wangu wapambane uwanjani tupate matokeo mazuri ili tuendelee kukaa kileleni katika msimamo wa Ligi hadi tutakaporejesha taji letu, huku tukiutazama mchezo wa Robo Fainali ASFC dhidi ya Geita Gold FC.” Amesema Nabi
Licha ya kutinga Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika ikifikisha alama 10, Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 65, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 57.