Kocha Mkuu wa Kikosi cha Young Africans Nasreddine Nabi, ametamba kuwa na wachezaji wenye kila sifa ya kuibuka na ushindi mzito dhidi ya Simba SC, Jumamosi (Desemba 11), Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Nabi amesema wachezaji wake wapo katika hali nzuri, huku wakiendelea na maandalizi ya mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki wa Soka kila kona ya nchi ya Tanzania.
Amesema hana budi kujivunia kuwa na kikosi imara msimu huu 2021/22, na anaamini wachezaji wake wote wana sababu ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza dhidi ya Simba SC ambayo itakua wenyeji katika mchezo huo.
“Tunaendelea kujiimarisha ili tuwe imara zaidi katika kila idara, ni mchezo ambao hutakiwi kufanya makosa, Simba ina wachezaji wenye uzoefu na uwezo, hivyo tunatakiwa kutowapa nafasi, kutofanya makosa,” Amesema Nabi
“Sina budi kusema kuwa nina wachezaji wazuri msimu huu, tunakwenda kupambana tukiwa na morari ya hali ya juu, hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha anapambana, ili tupate alama tatu Jumamosi.”
Young Africans bado inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania ikiwa na alama 19 baada ya kucheza michezo saba, huku Simba SC ikiwa nafasi ya pili kwa kumiliki alama 17.