Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Mohamed Nabi amesema ana uhakika Club Africain watatumia mbinu tofauti na ilivyokua kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa jijini Dar es salaam, Juma lililopita Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Young Africans leo itacheza mchezo wa Mkondo wa Pili ugenini Tunis-Tunisia ikiwa na deni la kusaka ushindi ama sare yoyote ya mabao ili kutinga Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Kocha Nabi amesema amewahusia wachezaji wake kucheza kwa nidhamu kubwa ili kuzishinda mbinu za wenyeji wao, ambao leo watacheza kwa nguvu kubwa ili kupata ushindi mbele ya Mashabiki wao.
“Tunatakiwa kuingia Uwanjani tukiwa na utulivu mkubwa tukiwa tunawaheshimu wapinzani wetu, ambao wataingia uwanjani kwa lengo la kushambulia ili wapate ushindi.”
“Kikubwa tunataka kuwazuia kucheza kwa nidhamu kubwa, kwa kuwa hatutaki kuwapa nafasi ya kukamilisha mashambulizi yao katika lango letu.”
“Nafahamu wanaweza kuwatumia wachezaji wao mawinga wenye kasi katika mchezo huu wa mkondo wa pili ambao nina uhakika hawakuwatumia kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Dar es salaam, nimebaini hilo na tayari nimewaelekeza watu wangu wa safu ya ulinzi namna ya kukabiliana nao.” amesema Kocha Nabi
Katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza hatua ya Mchujo uliopigwa jijini Dar es salaam Jumatano (Novemba 02), timu hizo zilitoka suluhu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.