Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi amekiri kuufuatilia mchezo wao dhidi ya TP Mazembe akiwa nyumbani kwake Ubelgiji jana Jumapili (April 02) huku wakishinda kwa bao 1-0 lakini akafichua kwamba usiku wa kuamkia jana aliota kuwa mfungaji wa bao hilo ni Farid Mussa.
Young Africans imemaliza kibabe michezo ya Hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika wakiifunga TP Mazembe kwa mara ya pili na kufikisha jumla ya alama 13 kileleni.
Nabi amesema baada ya kuota ndoto hiyo wakati wa mapumziko alishauriana na wasaidizi wake kumuingiza Farid mwanzo wa kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mudathir Yahya ambaye alimuona hakuwa katika kiwango bora katika dakika 45 za kwanza.
“Hii ni mara ya pili niliwahi kuota kama hivi kwa Mayele (Fiston) na alifunga ilikuwa msimu uliopita lakini sasa ni Farid ambaye hata mazoezini kabla ya kuondoka niliona ameongezeka ubora,”amesema Nabi.
“Nawapongeza sana wachezaji wangu na wasaidizi wangu kwa kusimamia malengo ya klabu yetu vizuri, nilitamani sana kushinda mchezo huu ni wajibu wetu kuwafanya mashabiki wetu wawe na furaha.” amesema Nabi
Baada ya kufanikiwa kufuzu Robo Fainali kwa kuongoza msimamo wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Mabingwa hao wa Soka Tanzania Bara Young Africans huenda wakakutana na mmoja wa miamba watatu kutoka ukanda wa Afrika Kaskazini au Magharibi.
Kikanuni Mshindi wa kwanza wa kila kundi atakutana na mshindi wa pili wa makundi mengine, hivyo kumalizika kwa michezo ya Hatua ya Makundi jana Jumapili (April 02), kumetoa nafasi ya kila timu shiriki katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kufahamu anaweza kukutana na nani.
Young Africans inaweza kukutana na Rivers United ya Nigeria, Pyramids ya Misri au USM Alger ya Algeria, ambazo zimemaliza katika nafasi ya pili katika makundi A, B na C.
Hata hivyo timu hizo zinapaswa kusubiri hadi keshokutwa Jumatano (April 05), ambapo Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ litachezesha Droo ya Robo Fainali ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho mjini Cairo Misri.
Wakati Young Africans ikisubiri Droo ya Robo Fainali, ndugu zao Simba SC nao wanasubiri Droo kama hiyo upande wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika huku ikitarajia kupangwa aidha na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Esperance de Tunis ya Tunisia na Wydad Casablanca ya Morocco.