Jeshi la Polisi mkoani Dodoma, Linamshikilia kwa mahojiano, Tito Machibya ‘nabii Tito’ ambaye amekuwa akionekana akitoa mafundisho, huku akiwa anakunywa pombe na kufanya vitendo ambavyo ni kinyume na maadili ya kidini kama kucheza nyimbo za taarabu akiwa kanisani kwake.
Hata hivyo Serikali imeeleza kuwa haimtambui nabii Tito, kwa kuwa hajasajili kanisa lake katika ofisi ya msajili wa taasisi za dini hapa nchini.
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Sheria wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Marlin Komba amesema.
‘’Ninachoweza kusema ni kwamba hakuna mtu anayezuiwa kuongea hapa nchini, mwache aongee anavyoweza ila Serikali imeshaona anachokifanya na yanayoendelea mitandaoni hatua zinachukuliwa dhidi yake’’.
Kwa upande wa viongozi mbalimbali wa dini wameonyesha kukerwa na kulaani vitendo anavyovifanya mtu huyo anayejiita nabii na kusema kuwa hakuna dini inayoruhusu mambo hayo.
Askofu msaidizi wa kanisa la kiinjili la kiluther Tanzania kkt, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Chediel Lwiza amesema kutokana na vitendo anavyovifanya mtu huyo hapaswi kujiita mtumishi wa Mungu.
Naye Msemaji wa Taasisi ya Kiislamu nchini, Rajab Katimba amesisitiza Serikali na viongozi wa dini kuingilia kati swala hilo na kueleza kuwa hakuna kitabu chochote cha dini kinachohamasisha ulevi na ukosefu wa maadili.