Klabu ya West Brom imekamilisha usajili wa mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Ublegiji Nacer Chadli akitokea Tottenham kwa ada ya Pauni milioni 13.

Chadli amekubali kusaini mkataba wa miaka minne wa kuitumikia klabu hiyo ya The Hawthorns na anaamiwa kuwa sehemu ya wachezaji ambao wataleta mabadiliko klabuni hapo kuanzia msimu huu wa ligi ya nchini England.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, alikua sehemu ya kikosi cha Spurs tangu mwaka 2013 aliposajiliwa akitokea FC Twente ya nchini Uholanzi kwa ada ya Pauni milioni 7, na alipokua kaskazini mwa jijini London alicheza michezo 119 na kufunga mabao 25.

Kabla ya kukamilika kwa taratibu za uhamisho wa Chadli, baadhi ya vyombo vya habari nchini England viliripoti kuwa, mshambuliaji huyo alikua katika harakati za kusajiliwa kwa mkopo, lakini baadae taarifa hizo zilibadilika na kuelezwa amesajiliwa moja kwa moja na klabu ya West Brom.

Meneja wa West Brom Tony Pulis amesifia usajili wa mshambuliaji huyo kwa kusema amepata mchezaji ambaye atasaidia mipango yake ya kufanya vyema msimu huu wa 2016/17 ambao unaonyesha utakua na kila aina ya ushindani.

“Ni mchezaji mwenye kiwango cha juu na mwenye uwezo wa kupambana wakati wote, ninaamini atanisaidia katika mipango yangu wa kufanikisha azimio la kufanya vyema kwa msimu huu,”

“Niliwahi kuzungumza juma lililopita kuhusu usajili huu, kwa sababu nina imani wachezaji wote waliojiunga nasi katika kipindi hiki wana viwango vya kupambana na Nacer ni mmoja wa watu ambao niliwatarajia.” Alisema Pulis

Chadli naye alizungumza baada ya kukamilisha usajili wake: “Ninahisi nipo katika mazingira salama. Nimekuja hapa kwa haraka zaidi tofauti na nilivyotarajia lakini kabla ya hapo nilizungumza na baadhi ya viongozi wa West Brom na nilithibitishia uwepo wa mipango mizuri iliyowekwa kwa ajili ya kusaka mafanikio.

Adrien Silva Athibitisha Kuihama Sporting Lisbon
Joe Hart Kufanyiwa Vipimo Vya Afya Mjini Turin-Italia