Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameelekeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kujenga kituo cha askari wa uhifadhi katika kijiji cha Namapuya na Namanja Wilayani Nachingwea ili kukabiliana na changamoto ya tembo wanaovamia makazi ya watu wakitokea Pori la Akiba Selous.
Ameyasema hayo leo alipofanya ziara ya kikazi ya kusikiliza kero za wananchi kuhusu changamoto za tembo wanaovamia makazi ya watu katika vijiji vya Namapuya na Namanja Wilayani Nachingwea Mkoani Lindi.
Aidha, ameelekeza kuwekwe mizinga ya nyuki katika shoroba ambazo tembo hao wanapita ili kuzuia wasifikie makazi ya watu.
Mhe. Masanja amewaasa wakazi wa maeneo hayo kuacha fikra za kutaka kuua tembo kwa sababu mnyama huyo analindwa na sheria za Kimataifa.
“Mkakati wa Serikali ni kuangalia namna wananchi wanaoathirika na tembo wanaweza kunufaika na rasilimali ya mnyama huyo kwa kuunda mfuko maalum” Mhe. Masanja amefafanua.
Katika ziara hiyo, Mhe. Masanja alitembelea familia iliyoathirika na tembo na kutoa mkono wa pole ambapo kijana wa familia hiyo, Riziki Issa aliuawa na tembo akiwa katika majukumu yake.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Mhe. Dkt. Amandus Chinguile ameishukuru Serikali kwa kuchukua hatua ya kutembelea eneo hilo lenye changamoto ya kuvamiwa na wanyama wakali na waharibifu kama tembo.
Awali, Mkazi wa Kijiji cha Namanja Binasa Tingo alitoa malalamiko kwamba kutokana na tembo kuingia kwenye makazi ya watu, wanashindwa kuendelea na shughuli za kila siku za shamba, kuchota maji n.k.
Mkazi wa Kijiji cha Namapuya, sais Ngololo ameongeza kuwa kufuatia tatizo la tembo kijijini hapo wananchi wamekuwa wakiishi kwa shida kwa kukoa chakula baada ya tembo kula mazao yao mashambani.