Wakati Yanga inaingia kambini leo Pemba, Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ hatakuwa tayari kwa mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Azam FC Machi 5, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa pia, Taifa Stars amesema kwamba anahitaji mechi tatu nyepesi ili aweze kuwa fiti kwa asilimia miamoja baada ya kupona mumivu yake.

Cannavaro alicheza mechi yake ya kwanza kwa dakika zote 90 Jumatano dhidi ya JKT Mlale baada ya kuwa nje tangu Novemba mwaka jana.

“Bado siko fiti, ila baada ya mechi yangu ya kwanza kucheza dakika zote na kwa jinsi ninavyofanya mazoezi, ninahitaji mechi tatu tu ili niwe fiti zaidi”alisema Cannavaro.

Akizungumzia kuhusu nafasi yake ndani ya timu hiyo Cannavaro alisema ushindani uliopo unawapa changamoto wachezaji wote kujituma zaidi ili kumshawishi kocha awape nafasi lakini kwa upande wake yeye ni mpambanaji na hata wachezaji wenzake wanalijua hilo.

“Tupo mabeki wanne wa kati na mwalimu ndio anajua amtumie nani katika mechi ipi, kwa hivyo mwenye kujituma ndiye atakayepewa nafasi,”alisema.

Yanga inapanda ndege leo kwenda kisiwani Pemba kesho kwa maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Azam FC Jumamosi ijayo.

Yanga imesonga mbele, Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afriuka kwa kuitoa kwa jumla ya mabao 3-0 Cercle de Joachim baada ya awali kushinda 1-0 katika mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita Mauritius.

Sasa mabingwa hao watetezi wanarudi kwenye vita ya Ligi Kuu, Machi 5 wakimenyana na washindani wao wakuu katika mbio za taji, Azam FC.

Zote, Yanga na Azam FC zina pointi 46 baada ya kucheza mechi 19 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara – lakini mabingwa watetezi wapo kileleni kwa wastani mzuri wa mabao (GD).

Mchezo wa Jumamosi umebeba taswira halisi ya nani atajiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa msimu huu na timu zote zimewekeza katika maandalizi mazuri ndani na nje ya Uwanja.

Azam FC wanakwenda Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ndege kucheza mchezo wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation kesho dhidi ya Panone Uwanja wa Ushirika.

Na Jumanne watarudi Dar es Salaam na moja kwa moja kuingia kambini katika hosteli zao za Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Chanzo: binzubeiry

Ajib Akabidhiwa Tuzo Ya Mchezaji Bora
Kompany Atoa Ya Moyoni Kuhusu 2014-15