Shirika lisilokuwa la kiserikali la Plan International mwaka 2016 lilifanya utafiti na kugundua kuwa nafasi ya watoto wa kike ulimwenguni haionekani machoni pa watu.

Hatua hiyo inatokana na sababu zinazoonesha kuwa takwimu zinazowahusu watoto wa kike ziko nyuma ya wakati, hazijakamilika na muda mwingine tafiti zake hazifanyiwi utekelezaji.

Tanzania imeonekana hakuna takwimu sahihi zinazoonyesha uhalisia wa changamoto anazozipata mtoto wa kike kutokana na ndoa za utotoni, hivyo kupelekea thamani ya mtoto wa kike kushuka katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo ambapo madhara yake yanaonekana baadae akiwa mtu mzima.

Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa Mtoto kutoka Shirika la Plan International–Tanzania, Jane Mrema amesema kiwango cha ndoa za utotoni kwa Tanzania kimefikia asilimia 36 ambacho ni kiwango kikubwa zaidi ya kiwango cha Dunia ambacho ni asilimia 34 na kwa hesabu za kimkoa ni asilimia 59 kwa kila mkoa.

“Hiyo ndio sababu kubwa iliyopelekea Shirika letu kuungana na Serikali pamoja na mashirika mengine kufanya utafiti huo wenye lengo la kufahamu vitu vinavyopelekea ndoa za utotoni pamoja na madhara yake baada ya ndoa hizo kutokea,”amesema. Jane.

Utafiti huo umefanyika kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yakiwemo ya Shirika la kutetea haki za watoto (Plan International), Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Shirika linalohusiana na Utafiti na maendeleo ya Afya ya Wanawake (FORWARD) pamoja na Shirika la Utafiti juu ya Kupunguza Umasikini (REPOA).

Aidha, baada ya utafiti huo kukamilika, iliandaliwa ripoti ambayo ilizinduliwa mnamo Machi, 2 mwaka huu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ripoti inayojulikana kama Ripoti ya Utafiti wa Visababishi na Madhara ya Ndoa za Utotoni Nchini Tanzania.

Vile vile, utafiti huo unaonesha kuwa Mkoa wa Mara wananchi asilimia 59 wanakubaliana na majibu ya utafiti huo ambapo mkoa wa Dar es Salaam asilimia 56, mkoa wa Dodoma asilimia 53, mkoa wa Lindi asilimia 52 na mkoa wa Tabora asilimia 51.

Sababu nyingine ya ndoa za utotoni ni mtazamo wa tamaduni, mila na desturi baina ya jamii mbalimbali kuhusu miaka ya mtoto wa kike anayetakiwa kuolewa, unyago, ukeketaji pamoja na ngoma za asili zinazopelekea watoto kuozwa mapema.

Hata hivyo,  tafiti hizo zinaonyesha kwamba maeneo ya vijijini asilimia 18 ya wanawake wamekeketwa wakati Mijini ni asilimia 7 na Mikoa inayoongoza ni Manyara asilimia 81, Dodoma asilimia 68, Arusha asilimia 55, Singida asilimia 43 na Mara asilimia 38.

 

Rais Magufuli aiagiza Tanesco kukata umeme kwa Wizara zenye madeni
Video: Meya wa Kinondoni azindua mashindano ya mpira Kata ya Msasani