Nahodha wa timu ya taifa ya China Zheng Zhi, amefungiwa kucheza michezo minne ya ligi ya nchini humo, baada ya chama cha soka (CFA) kumkuta na hatia ya utovu wa nidhamu.
Zhi alifikishwa kwenye kamati ya nidhamu ya chama cha soka nchini China, kufuatia kosa alilolifanya la kuwashawishi wachezaji wenzake kukataa kuwapa mkono wachezaji wa timu pinzani mwishoni mwa juma lililopita.
Zheng, ambaye ana sifa ya kukiongoza kikosi cha Guangzhou Evergrande katika micka sita ya mafanikio ya kutwaa ubingwa wa China, pia ametozwa faini ya Yuan 40,000 sawa na dola za kimarekani 6,000, huku klabu kwa ujumla ikitozwa faini ya Yuan 100,000 kwa kushindwa kuwazuia wachezaji wao kutofanya kitendo hicho cha utovu wa nidhamu.
Katika mchezo huo Guangzhou Evergrande walikubali kichapo cha mabao manne kwa matatu kutoka kwa Tianjin Quanjian.
Wachezaji wenginwa wa Guangzhou Evergrande kama Mei Fang, Feng Xiaoting, Paulinho, Ricardo Goulart, Wang Shangyuan, Zeng Cheng, Zou Zheng, Huang Bowen, Yu Hanchao na Zheng Long kila mmoja ametozwa faini ya Yuan 10,000.
Adhabu hiyo kwa Zheng inakuwa ya pili kwa msimu huu, kwani aliwahi kuadhibiwa kwa kufungiwa michezo miwiwli mwezi Machi kwa kosa la kuonyeshwa kadi nyekundu.
Adhabu nyingine ilizotangazwa na kamati ya nidhamu ya CFA imemuhusu mchezaji kutoka nchini Uturuki na klabu ya Beijing Guoan Burak Yilmaz ambaye amefungiwa michezo mitano na kutozwa faini ya Yuan 25,000, kwa kosa la kumsukuma kwa makusudi mchezaji wa Jiangsu Suning wakati wa mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita uliomalizika kwa sare ya bila kufungana.
Kiungo kutoka nchini Brazil na klabu ya Shanghai SIPG Oscar, naye ameadhibiwa kwa kufungiwa michezo minane kwa kosa la kutoa lugha chafu dhidi ya muamuzi, huku mbrazil mwenzake Hulk, Wu Lei na kocha wao Andre Villas-Boas wakifungiwa michezo miwili kila mmoja kwa kitendo cha kuunga mkono utovu wa nidhamu ulioonyeshwa na kiungo huyo wa zamani wa mabingwa wa soka nchini England Chelsea.