Imedaiwa kuwa mtu aliyekuwa anaendesha MV Nyerere katika siku ambayo chombo hicho kilizama hakuwa na elimu ya kiwango cha kutosha kufanya kazi hiyo.

Alan Mahatane, ambaye alifariki katika ajali hiyo anadaiwa kuiendesha MV Nyerere akiwa na kiwango cha elimu cha Deck Ratings ambayo haikidhi kiwango cha elimu iliyokuwa inastahili kwa nahodha husika ambayo ni kuanzia Master Near Coast Deck Office Class 4.

Akizungumzia elimu ya marehemu, Salum Adam ambaye ni baharia wa meli ya MV Nyehunge aliyeeleza kuwa amesoma naye, amekaririwa na Mwananchi akieleza kuwa kiwango cha elimu alichokuwa nacho hakimruhusu kuendesha meli hiyo bila kuwa na uangalizi wa karibu wa Nahodha mwenye sifa kamili.

Hata hivyo, walipoulizwa kuhusu suala hilo kwa nyakati tofauti, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Jonathan Shanna na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella walisema hawawezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa hadi uchunguzi kamili utakapokamilika.

Aidha, Mongella alisema kuwa katika utaratibu wa watu watakaohojiwa ni pamoja na fundi mkuu wa kivuko hicho, Alphonce Charahani ambaye aliokolewa kufuatia jitihada za saa 48.

MV Nyerere ilizama Septemba 20 mwaka huu katika Ziwa Victoria na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 200.

 

Harmorapa apata ‘mtetemo’ kumgusa Wema
Tetemeko lachukua maisha ya mamia