Chama cha Soka Misri “EFA” kimefanya uamuzi wa kumsimamisha kucheza soka nahodha wa Zamalek, Mahmoud Abdelrazek ‘Shikabala’ kwa miezi nane pamoja na kumtoza faini ya LE 500,000 kutokana na utovu wa nidhamu.
Zamalek ilibeba taji lao la 13 la ligi siku ya Ijumaa usiku baada ya kutoka sare na Bank Al Ahly katika mechi yao ya mwisho ya msimu.
Matokeo ya mchezo huo yalikuwa ya machafuko baada ya rais wa EFA, Ahmed Megahed kukataa kukabidhi vizuri kombe kwa Zamalek, kitendo ambacho kilisababisha sherehe isiyo na mpangilio mzuri sana.
Baadaye iliripotiwa kwamba nahodha wa The White Knights, Shikabala alikuwa na ugomvi na Megahed, ambaye aliwajuza polisi kutowaruhusu wachezaji wengine wa Zamalek, ambao walikuwa nje ya kikosi cha mechi, kuingia uwanjani kusherehekea na wachezaji wenzao.
Pia Shikabala alionekana baada ya mchezo huo akiwaongoza wachezaji wenzake, wakiimba matusi kuwaelekeza Al Ahly na mashabiki wao.
Kufuatia matukio hayo, Shirikisho la Soka la Misri liliamua kuwaadhibu wachezaji wawili wa Zamalek kwa sababu ya utovu wa nidhamu, pamoja na nahodha wao Shikabala.