Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amewatembelea Makocha ambao wapo kwenye mafunzo ya ngazi ya Diploma ya Ualimu wa Michezo Daraja A inayotambuliwa na Shirikisho la Mpira Afrika (CAF) yanayoendelea katika Kituo cha Michezo Tanga kinachosimamiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Naibu Waziri Mwinjuma amefanya ziara hiyo Juni 12, 2023 jijini Tanga na kukutana na Waalimu hao na kuwasisitiza kutumia fursa hiyo vema ili kujiongezea maarifa ambayo yatasaidia kuinua michezo nchini na kuibua vipajji vya wanamichezo katika maeneo wanayotoka.
Naye Rais wa Shirikisho la Mpira Tanzania Bw. Wales Karia amesema Kozi hiyo ni ya juu na inatambuliwa na CAF na Tanzania ni nchi iliyopewa heshima ya kutoa mafunzo hayo.
Kwa upande wake mmoja wa walimu ambao wanapata mafunzo hayo Juma Kaseja kutoka timu ya Kagera Sugar amesema mafunzo hayo ni mazuri, wanapata elimu ya juu katika mpira wa miguu Afrika ambayo wataitumia kwa manufaa ya timu wanazofanya kazi pamoja na Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Mafunzo hayo yanawahusisha walimu wa mpira kutoka Zambia, Zimbabwe, Rwanda, Somalia na wenyeji Tanzania.